Sunday, July 12, 2009

ONGEZEKO LA WATOTO W MITAANI_BOMU LINALOSUBIRI KULIPUKA

Na Gebo Arajiga,Arusha

Arusha ni miongoni mwa mikoa 26 ya Tanzania iliyoko kaskazini mwa Tanzania ikiwa imejaliwa kuwa na madini mbalimbali,hifadhi za wanyama ambazo kila mwaka watalii wengi huja kutembelea na kushuhudia maajabu hayo baadhi ya mbuga hizo ni Hifadhi ya Manyara ambapo ni sehemu pekee ya ndege aina ya flamingo hutaga mayai yao,Olduvai gorge sehemu alipovumbuliwa binadamu wa kwanza na Ngorongoro crater moja kati ya maajabu saba ya dunia aidha pia mkoa huu ni makao makuu ya jumuia ya Afrika Mashariki(EAC) lakini wakazi wa mkoa huu wengi wao ni wakipato cha chini.

Ilifikia hatua hata rais wa wa zamani wa marekani Bill Cliton alipoitembelea Tanzania aliifananisha hali ya mkoa huu kuwa ni Geneva ya Afrika lakini kutokana na sifa yote hiyo bado mkoa huu unasumbuliwa na tatizo la watoto wa mitaani au watoto wa Utuli na umaskini wa kipato miongoni mwa jamii.


Ingawa mkoa huu kuwa na vivutio vingi vya utalii na kuingizia fedha nyingi za kigeni lakini hali ya kipato kwa wananchi bado ni mbaya hali ya umaskini katika mkoa huu ipo hatua chache kutoka katikati ya mji katika maeneo yenye msongamano wa watu wengi kama vile Ngarenaro,Esso,Unga Ltd ambapo biashara ya kujiuza na matumizi ya madawa ya kulevya imekuwa kitu cha kawaida ili kujiongezea kipato.


Lakini pindi unapofika kwa mara ya kwanza mkoa hapa utashangaa na hali utakayokuta nayo watoto wanaozurura na kuomba fedha kwa kila mtu anayekutana naye,barabara zake ni finyu na mbovu zisizofaa .


Tatizo la watoto wa mitaani ambao wengi wao ni wenye umri wa kuwepo shuleni lakini kutokana na matatizo yanayowakabili wameshindwa na kuamua kuja mjini kutafuta kipato ili waweze kujikomboa kiuchumi.

WANANCHI mbalimbali wa mjini Arusha ambao walihojiwa na Jambo leo wameitaka Manispaa ya Arusha kufanya jitihada za makusudi kuwaondoa watoto wa mitaani waliozagaa katikati ya mji wa Arusha na kuwa kero kubwa wananchi kwa kuwaibia mali zao pamoja na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya pamoja na gundi ambayo huyafanya hadharani bila kificho na kuwarudisha makwao au watunzwe na kupata nafasi ya kusoma.



Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi hao walisema kuwa watoto hao wamekuwa na tabia ya kuomba fedha kwa wapita njia na pindi wanaponyimwa wamekuwa wakiwatukana na kuwachukulia kitu chochote kinguvu na kukimbia huku wakitishia kwa bisibisi na visu.



Walter Taluka mkazi wa Sakina mjini hapa alisema kuwa tatizo la watoto wa mitaani kwa sasa mkoani hapa linazidi kushamiri kutokana na hali ngumu ya kimaisha katika familia zao”Hii ni aibu kubwa sana kwa mkoa kama huu wenye utajiri wa kila aina kuwa na idadi kubwa ya watoto wa mitaani huku wakihusishwa na matumizi ya madawa ya kulevya.



Naye mkazi wa kijiji cha Kiranyi Nashuma Samweli diwani mstaafu alisema kuwa “imefika muda sasa serikali ya mkoa ikaingilia kati kuwanusuru watoto hawa ambao wanaharibika kwa matumizi ya madawa ya kulevya na kutegemea kuomba ili waweze kuendesha maisha yao wengi wao hubakana haya mambo yapo katika makundi yao sasa hapa tunalea taifa gani jamani wachukuliwe na kurudishwa makwao au serikali ichuku jukumu la kuwalea katika vituo”alisema diwani huyo mstaafu



Wengi wa watoto hao ni wenye umri kati ya miaka kumi hadi kumi na nane umri ambao wanapaswa kuwepo shuleni lakini kutokana na umaskini wa familia na wao kuamua kukimbia nyumbani kuja mjini na kujitafutia ridhiki.



Moja wa watoto wa mitaani James John anasema kuwa yeye anatokea katika mji mdogo wa Magugu mkoani Manyara na aliamua kuja mjini kujitafutia maisha kwa kuchoka hali ngumu ya maisha waliyokuwa nayo wazazi wake na kipigo alichokuwa akipewa na baba yake mzazi pindi anapokuwa amelewa.



"Niliamua kukimbia nyumbani kuepuka adhabu za mara kwa mara alizokuwa akinipa baba na kuamua kuja hapa Arusha”alisema mtoto huyo.



Tatizo la watoto wa mitaani katika mkoa wa Arusha linazidi kushamiri mkoani hapa huku watoto hao wakijihusisha na matumizi ya bangi,gundi na madawa mengine ya kulevya.



Watoto hao hulala katika mabaraza ya maduka makubwa yaliyopo katikati ya mji na wengine hulala katika eneo la stendi ndogo ya magari na ndani ya makaravati ya barabarani.



MWISHO.

No comments:

Post a Comment